KAMATI ya Sheria na hadi kwa wachezaji ya Shirikisho la soka Tanzania (TFF) imebariki maamuzi ya kamati ya masaa 72 ya Shirikisho hilo kuipa Simba pointi tatu dhidi ya Kagera Sugar.
Kwa takriban wiki mbili sasa kumekuwa na mgogoro wa pointi ambazo kamati ya masaa 72 iliipa Simba baada ya kushinda rufaa yao ya kupinga Kagera Sugar kumtumia mchezaji Mohamed Fakhi aliyekuwa na kadi tatu za njano katika mechi dhidi yao iliyochezwa kwenye uwanja wa Kaitaba, Bukoba ambapo Simba ilifungwa mabao 2-1.
TFF ililipeleka sakata hilo kwenye kamati ya Sheria na hadhi kwa wachezaji iliyo chini ya Richard Sinamtwa baada ya Kagera kuomba marejeo ya hukumu yao wakidai Fakhi alikuwa na kadi mbili za njano na si tatu kama inavyodaiwa na Simba na ilivyoamuliwa na kamati ya masaa 72.
Tangu juzi gazeti hili linatambua kwamba kamati ya Sinamtwa baada ya kufanya mahojiano na wahusika kadhaa kutoka Kagera, Simba, African Lyon (mechi ambayo Fakhi anadaiwa alipata kadi) na maofisa wa bodi ya ligi ilibaini mchezaji huyo kuwa na kadi tatu za njano kabla ya mechi ya Simba na hivyo maamuzi ya kamati ya masaa 72 yatabaki kama yalivyotangazwa.
Habari za uhakika kutoka ndani ya kamati hiyo zinasema kuna madudu mengi yalifanyika katika suala hilo likihusisha baadhi ya maofisa wa bodi ya ligi wanaohusika na utunzawaji kumbukumbu za ligi.
“Kamati haitaweza kuwaachia, lazima ichukue hatua ili wajifunze iwe fundisho,” alisema mtoa habari wetu. Naye mwenyekiti wa kamati hiyo Sinamtwa alisema ukweli wote atauzunguza leo juu ya sakata hilo kwa vile kumekuwa na uhuni mwingi katika uendeshwaji wa tukio zima.
Simba ndio inaongoza ligi ikiwa na pointi 62 na imebakiza mechi tatu kumaliza ligi huku Yanga inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kwa pointi 56 ikiwa na mechi tano kibindoni.

Tupia Comments: